NIDA yaja na mfumo mpya wa uombaji vitambulisho

0
122

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imetambulisha Mfumo wa Usajili wa watu kwa njia ya mtandao utakaowezesha wananchi wenye sifa za kuomba vitambulisho vya Taifa kwa kujaza fomu mtandaoni mahali popote bila kulazimika kufika katika ofisi za NIDA.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano (NIDA), Geofrey Tengeneza amesema ili kujisajili mwombaji ataandika eonline.nida.go.tz katika mtandao wa internet na kufuata maelekezo.

“Mfumo huu unalenga kupunguza usumbufu kwa waombaji wa vitambulisho vya Taifa ambao kwa sasa wanalazimika kufika ofisi za NIDA kuchukua fomu za maombi ya vitambulisho vya Taifa kwani kupitia mfumo huu ujazaji wa fomu na kuweka viambatisho utafanyika mahali popote kwa kutumia kifaa chenye uwezo wa kupokea mtandao wa mawasiliano,” amesema Tengeneza.

Amesema baada ya kujaza fomu, mwombaji atatakiwa kuchapa fomu (print) na kuipeleka fomu yake ofisi za NIDA iliyoko katika wilaya anayoishi akiwa na nakala ngumu za viambatisho alivyopakia katika mfumo ili kukamilisha utaratibu wa usajili kama vile kuhojiwa na uhamiaji, kupigwa picha na kuchukuliwa alama za vidole.

Kwa upande wake Meneja Usajili na Utambuzi (NIDA), Julien Mafuru amesema kumekuwa na malalamiko ya kukosewa kwa taarifa za uombaji vitambulisho hivyo kupitia mfumo huu utasaidia kupunguza kero hiyo kwani mwombaji atajaza taarifa zake mwenyewe.

Amesema wanaenda kupanua wigo wa kuwaandikisha Watanzania ambao watakuwa nje ya nchi kwa hiyo na wenyewe watapata faida ya kujaza fomu moja kwa moja kwenye mtandao.