Nida Textile yakumbana na rungu la Waziri Jafo

0
171

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Selemani Jafo ametoa muda wa mwezi mmoja na nusu kwa kiwanda cha Nida Textile kinachotengeneza bidhaa za nguo, kuhakikisha kinarekebisha mfumo wa majitaka ili uendane na sheria na kanuni za utunzaji wa mazingira.

Waziri Jafo ametoa muda huo mara baada ya kutembelea viwanda vya Nida Textile na Royal Soap Detergent vilivyopo mkoani Dar es Salaam.

Wakati wa ziara yake, Waziri Jafo amebaini viwanda hivyo vinaathiri mazingira kwa kutiririsha maji taka na kuvusha moshi, na hivyo kuathiri wakazi wa eneo la Mabibo.

Wakazi wa eneo hilo la Mabibo wamemweleza Waziri Jafo kuwa kwa muda mrefu viwanda hivyo viwili vimekuwa havifuati sheria na kanuni za mazingira, na wameishukuru Serikali kwa kuingilia kati suala hilo.

Waziri Jafo amesema Serikali imekuwa ikihamasisha uwekezaji wa viwanda nchini, lakini amewataka wamiliki wa viwanda vyote kutekeleza sheria na kanuni za utunzaji wa mazingira.