NHIF yafafanua toto afya kadi

0
219

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bernard Konga ametolea ufafanuzi taarifa iliyotolewa na mfuko huo Machi 13, 2023 kuhusu utaratibu wa bima ya afya ya Toto Afya Kadi.

Katika taarifa yake hapo jana, NHIF ilitangaza kuwa watoto ambao awali walikuwa wakisajiliwa kupitia utaratibu wa bima ya afya ya Toto Afya Kadi, sasa watasajiliwa kupitia vifurushi vya bima ya afya au shule wanazosoma.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa NHIF inafanya maboresho ya usajili na huduma kwa watoto waliokuwa wanasajiliwa kupitia utaratibu wa bima ya afya ya Toto Afya Kadi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Konga amesema katika kipindi hiki cha maboresho, wazazi wanashauriwa kusajili watoto wao kama wategemezi kupitia vifurushi vya bima ya afya au kupitia shule wanazosoma.

Amesema kama Baba hana bima sasa anaruhusiwa kukata, ili amjumuishe na mwanawe katika bima hiyo.

“Sasa hivi wanaruhusiwa kukata bima itakayojumuisha familia, tuna kifurushi kinaruhusu familia, kwa wale watoto ambao hawajaanza shule maana yake wapo kwenye mpango wa Serikali wa matibabu bure, hivyo hao hawatalazimika kuwa na bima lakini kwa wale walioanza shule wawe na bima.” amesisitiza Mkurugenzi Mkuu huyo wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya