NHC kujenga Majengo ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

0
145

Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo imesaini mkataba wa ujenzi wa jengo la Wizara hiyo kwa awamu ya pili lenye ghorofa sita na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) jingo litakalojengwa eneo la Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.

Akizungumza katika hafla hiyo ya utiaji saini leo Septemba 22, 2021 jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dkt. Hassan Abbasi amesema jengo hilo litakuwa na ofisi za kisasa pamoja na mahitaji yote yanayohusika katika sekta za Sanaa, Utamaduni na Michezo.

“Jengo hili litakuwa la kihistoria kwa kuwa Wizara hii haijawahi kumiliki jengo la hadhi hii, matarajio yetu jengo hili litakuwa kichocheo cha sekta hizo kutoa huduma bora na stahili kwa wadau wa sekta na wanananchi kwa ujumla” amesema Dkt. Abbasi.

Aidha, Dkt. Abbasi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa jengo hilo ambazo ni shilingi Bilioni 22.843 huku ujenzi huo ukitarajiwa kukamilika ndani ya miezi 24.

Katibu Mkuu Dkt. Abassi amewahimiza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambao ni watekelezaji wa mradi wa ujenzi wa jengo hilo pamoja Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambao ni wasanifu na wabunifu wa majengo hayo wakamilisha mradi huo kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa kwa kuwa wao ni mabingwa wameaminiwa kwa uzoefu wao katika masuala ya ujenzi.