Nguruwe wenye thamani ya milioni 370 wamekufa kwa homa, Serikali yaweka mikakati kudhibiti

0
188

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha ugonjwa wa homa ya Nguruwe ulioikumba Mikoa ya Kanda ya Ziwa hivi karibuni unadhibitiwa, huku akisema kuwa tangu ugonjwa huo uanze mpaka sasa umeshasababisha vifo vya Nguruwe 1500 wenye thamani ya shilingi milioni 375.

Ndaki ameyasema hayo jijini Dodoma alipokuwa akiongea na Waandishi wa Habari kuhusu hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kuudhibiti ugonjwa huo uliokumba Mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Amesema kuwa vifo hivyo vimesababisha hasara ya moja kwa moja kwa wafugaji kwa sababu kipato hicho kilichopotea ilikuwa wakipate wafugaji huku akiwataka wafugaji hao kuwa watulivu na kufuata maelekezo ya serikali ili ugonjwa huo uweze kudhibitiwa kwa haraka.

Ameongeza kuwa ugonjwa huo unaosababishwa na virusi unahama kutoka kwa nguruwe pori na Ngiri na unasambaa kupitia njia ya Maji, Damu au Kinyesi.

“Tumeongeza Wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wakala ya Maabara ya Veterinari (TVLA), Wataalamu kutoka Chuo cha SUA na Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) kwenda kuungana na wataalamu wa Halmashauri ili kuongeza nguvu ya kudhibiti ugonjwa huo,” amesema Ndaki

Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa, Hezron Nonga amesema kuwa ili ugonjwa huo usisambae zaidi ni muhimu wafugaji kuhakikisha kuwa mifugo yao inakuwa katika mabanda wakati wote na kuacha kusafirisha mifugo na mazao yake kutoka sehemu moja kwenda nyingine kabla ya kupimwa na Daktari.