NECTA yafuta matokeo kwa baadhi ya shule

0
2461

Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetangaza kufuta matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi uliofanyika tarehe Sita na Saba mwezi Septemba mwaka huu katika shule zote za msingi za halmashauri ya Chemba mkoani Dodoma.

Shule nyingine za msingi zilizofutiwa matokeo hayo ni Hazina na New Hazina zilizopo katika manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es salaam, Aniny Nndumi na Fountain Joy za Ubungo jijini Dar es salaam, shule za msingi za Alliance, New Alliance na Kisiwani za mkoani Mwanza, pamoja na Kondoa Integrity iliyopo wilayani Kondoa mkoani Dodoma.

Katibu Mtendaji wa NECTA, Dkt Charles Msonde amesema kuwa Baraza hilo limefikia uamuzi huo kutokana na kuwepo kwa vitendo vya wizi na uvujaji wa mitihani hiyo vilivyofanywa na baadhi ya watumishi waliopewa dhamana ya kuilinda mitihani hiyo, vitendo vilivyobainika katika shule na vituo vya kufanyia mitihani.

Dkt Msonde amesema kuwa kufuatia kufutwa kwa matokeo ya mtihani huo, mitihani ya shule zote zilizofutiwa matokeo itarejewa tarehe Nane na Tisa mwezi huu.

Ameongeza kuwa NECTA pia imefuta vituo vya mitihani vya shule za msingi za Hazina, New Hazina, Aniny Nndumi, Fountain Joy, Alliance, New Alliance, Kisiwani na Kondoa Integrity hadi hapo Baraza la Mitihani Tanzania litakapojiridhisha kuwa havitakiuka tena kanuni za mitihani.

Tayari NECTA imeziarifu mamlaka za ajira na za usimamizi wa sheria kuwachukulia hatua kali watumishi wote na mtu yeyote aliyebainika kujihusisha na kuvujisha mtihani huo kwa mujibu wa kanuni za utumishi na sheria za nchi.