Wananchi na viongozi mbalimbali wamejitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi mkuu unaoendelea Tanzania kote ambapo wanachagua rais, wabunge na madiwani watakaoongoza kwa miaka mitano.
Kwa upande wa Chama cha Mapinduzi (CCM), mgombea urais wa chama hicho, Dkt. Magufuli akiwa ameambatana na mkewe, Janeth Magufuli wamepiga kura katika kituo cha Idara ya Maji Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma.
Msimamizi wa kituo hicho, Abdallah Said amesema upigaji kura umeenda vizuri huku Dkt. Magufuli akiwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kuwachagua viongozi bora ambao watalitumikia Taifa katika kuleta maendeleo.
Huko visiwani Zanzibar, mgombea wa urais kupitia Chama cha Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi amepiga kura katika Jimbo Kwahani huku mgombea mwenza wa urais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akipiga kura katika Jimbo la Kiembe Samaki.
Aidha, mgombea urais wa Zanzibar kupitia ACT-Wazalendo amepiga kura katika kituo cha Garagara kisiwani Unguja, huku pia wagombea wengine wa vyama vya AAFP, ADC, CUF nao wakitimiza haki yao ya kikatiba.
Wakati wananchi katika maeneo mbalimbali nchini wakiendelea kupiga kura, TBC imeshughudia wananchi katika maeneo kadhaa nchini wakiendelea kupiga kura huku wakiipongeza tume ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kwakuratibu vyema zoezi la upigaji kura linaloendelea kwa amani.
Fuatilia TBC1 na ukurasa wetu wa YouTube (TBCOnline) kwa matangazo mbashara ya zoezi la upigaji kura linavyofanyika nchi nzima.