NEC wapewa kongole

0
351

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Dkt Athumani Kihamia ameeleza kuridhishwa na utendaji kazi wa watumishi wa tume hiyo kutokana na kufanya kazi kwa bidii, ushirikiano, weledi na uzalendo.

Dkt Kihamia ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam alipokutana na wafanyakazi wa  NEC kwa lengo la kujadili mambo mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa majukumu ya Tume hiyo.

Amesema kuwa katika kipindi alichokaa NEC amegundua kuwa utendaji kazi wa mazoea umepungua,  na watumishi wengi wamekuwa wakitekeleza majukumu yao kwa wakati, kwa uaminifu, kutunza siri na kuepuka matumizi ya fedha yasiyo ya lazima.

Kwa mujibu wa Dkt Kihamia, kwa sasa NEC imeimarika vya kutosha kwa kuwa wakati alipofika wastani wa utendaji kazi ulikuwa asilimia 52, ikimaanisha kuwa zaidi ya asilimia 48 ya watumishi walikuwa hawawajibiki ipasavyo, lakini sasa uwajibikaji umefikia wastani wa asilimia 65 baada ya kuwekeana malengo.

“Kwa hiyo tulipo sasa tupo juu ila ni lazima tuendelee kuwa kitu kimoja,  ingawa katika kuimarika huko wapo wenzetu wachache sana wenye matatizo madogo madogo, hivyo wanatakiwa warekebishwe” amesisitiza Dkt Kihamia.