Nchi za SADC zatakiwa kuungana kutokomeza Malaria

0
237

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amewataka Mawaziri wa Afya kutoka nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuungana ili kutokomeza ugonjwa wa Malaria.

Akizungumza Kibaha mkoani Pwani wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Zero Malaria inaanza na Mimi kwa nchi za SADC, Waziri Ummy Mwalimu amesema kuwa, mapambano dhidi ya Malaria yanahitaji jitihada za pamoja za nchi hizo.

Waziri Ummy ameongeza kuwa, jitihada zinazofanywa na Tanzania zinapaswa kuwa katika kila nchi ili kutokomeza kabisa ugonjwa huo katika Ukanda wa SADC.

Amefafanua kuwa, maambukizi ya ugonjwa wa Malaria yamekua yakiongezeka katika nchi za SADC, ambapo katika kipindi cha mwaka 2018 watu Milioni 50 walipata maambukizi ya ugonjwa huo.

Hata hivyo Waziri Ummy Mwalimu amewataka Mawaziri wenzake wa Afya kutoka nchi za SADC, kutumia dawa za Viuwadudu wa Malaria kutoka katika kiwanda cha Tanzania Biotech Product cha hapa nchini ili kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo.