Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kamandi ya Wanamaji (NAVY) limeendelea kuboresha utoaji huduma za afya katika hospitali yake ya kikosi cha NAVY iliyopo Kigamboni mkoani Dar es salaam, baada ya kufanikiwa kupanua jengo la kutolea huduma za mama na mtoto (RCH).
Upanuzi wa Jengo hilo utasaidia upatikanaji wa huduma za mama na mtoto pamoja na upasuaji kwa akina Mama Wajawazito wanaokwenda kupatiwa huduma katika hospitali hiyo.
Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Wanamaji Meja Jenerali Richard Makanzo amesema, jengo hilo likikamilika litasaidia familia za askari na Wananchi wa Kigamboni kupata huduma bora za afya za mama na mtoto.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa tiba wa JWTZ Kanali Albert Kitumbo amesema kuwa, ujenzi wa jengo hilo utaongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za mama na mtoto.
Naye Mganga Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Wanamaji Meja Seth Mwasambogo ameeleza kuwa wameamua kejenga jengo la mama na mtoto katika hospitali hiyo ili kuboresha upatikanaji wa huduma hizo kwa familia za askari na Wananchi wa Kigamboni.
Kwa sasa hospitali hiyo ya kikosi cha NAVY inapokea akina mama Wajawazito 100 wapya kila mwezi na wagonjwa 50 wanaojirudia, huku ikiwa haina uwezo mkubwa wa kutoa huduma za mama na mtoto kutokana na ufinyu wa majengo.