NARCO yaja na mkakati wa kujiendesha kibiashara

0
142

Meneja Mkuu wa Kampuni za Ranchi za Taifa (NARCO), Prof. Peter Msoffe ametaja mikakati itakayosaidia kampuni hiyo kuweza kujiendesha kibiashara zaidi ikiwa ni pamoja kujiimarisha katika uzalishaji wa nyama ya kutosha iliyo bora, uzalishaji wa mifugo iliyo bora, kutoa mafunzo kwa wataalam na wafugaji, kujiendesha kibiashara na kuweza kupeleka gawio serikalini.

Prof. Msoffe ameibainisha mikakati hiyo baada ya kumalizika kwa kikao cha makabidhiano ya ofisi na aliyekuwa Kaimu Meneja Mkuu wa NARCO, Masele Shilagi kilichofanyika kwenye ofisi hizo jijini Dodoma.

Kwa upande wake Shilagi ambaye amesema kampuni imekuwa ikiendelea kuimarika kimapato ambapo iliweza kujiendesha bila kutumia ruzuku kutoka serikalini. Pia wameweza kusimamia mapato na matumizi ambapo kampuni imekuwa ikipata hati safi.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Uzalishaji na Masoko, Stephen Michael amesema kuwa viongozi na watendaji wanao wajibu wa kujipanga vizuri ili kuhakikisha malengo na matarajio ya serikali yanatimizwa. NARCO inazo fursa nyingi kwenye uzalishaji wa nyama bora, mifugo bora, malisho na utoaji wa elimu kwa wafugaji.

Lakini pia amewashauri waangalie namna bora ya kushirikiana na sekta binafsi lengo likiwa ni kuongeza uzalishaji na kuongeza mapato.