Naibu Waziri Masanja: Wakuu wa wilaya simamieni mipaka ya hifadhi

0
261

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amewataka wakuu wa wilaya nchini kusimamia vema maeneo ya hifadhi, ili kuepusha migogoro baina ya shughuli za kibinadamu na hifadhi.

Akizungumza wakati wa ziara ya mawaziri wa kisekta ya kutatua migogoro katika vijiji 975 nchini Masanja amesema, “Kila mtu akisimamia eneo lake vizuri hii migogoro itapungua sana ama kuisha lakini tukisubiri Serikali iseme au kamati ya mawaziri iseme, maeneo ya hifadhi yatakwisha.”

Amefafanua kuwa changamoto kubwa inayoipata Serikali kwenye uhifadhi ni muingiliano wa shughuli za kibinadamu na utunzaji wa maeneo ya hifadhi, ambapo wananchi wanaanzisha vijiji katikati ya hifadhi.

Kufuatia hali hiyo Naibu Waziri Masanja amewataka wakuu wa wilaya kuwahakiki wahamiaji wanaoingia katika maeneo yao, ili kujua sababu inayowafanya waanzishe vijiji katika hifadhi.

Pia amewataka watoe maelekezo ya kutosha kwa wananchi kuhusu umuhimu wa uhifadhi na kuwasimamia, hatua itakayosaidia kuondokana na migogoro ya ardhi.

Naibu Waziri huyo wa Maliasili na Utalii ameongeza kuwa endapo hifadhi zitaendelea kuvamiwa, changamoto za mabadiliko ya tabianchi zitaendelea kujitokeza.