Naibu Spika wa Bunge Mussa Zungu ameishauri wizara ya Maji kuboresha mchakato wa umiliki wa visima kwa kuwarudishia Wananchi visima walivyovichukua, ili huduma ya maji iendelee kupatikana.
“Hivi visima toka mchukue mmefanya tathimini ya ufanisi wake?. Visima vyote vya Wananchi ambavyo DAWASA mmevichukua vimekufa… mnawapa tabu Wananchi, mmejiongezea mzigo for nothing. Tunaomba mfikirie upya namna ya kurudisha visima kwa Wananchi vifanye kazi.” Ameshauri Naibu Spika Zungu
Ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma baada ya Mbunge wa jimbo la Temeke mkoani Dar es Salaam, Dorothy Kilave kuhoji kwanini Serikali isiwarudishie Wananchi visima maana tangu vimechukuliwa hakuna marekebisho na Wananchi wanaendelea kukosa maji.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema, visima hivyo vilichukuliwa kwa sababu za kiufundi na havitarudishwa kwa Wananchi.
“Visima vimechukuliwa kwa sababu za kiufundi, sasa hivi kwa mfano wizara ya Afya inaweza kumiliki hosipitali zake na sisi wizara ya Maji tunahitaji kumiliki vyanzo hivi vya maji vyote ili viwe chini ya uangalizi wa watalaam wetu, hatutavirudisha kwa Wananchi bali tutaongeza nguvu ili kuhakikisha vinakwenda kutumika na kuongeza usambazaji wa maji kwa Wananchi.” Amesema Naibu Waziri Maryprisca Mahundi