Spika wa Bunge, – Job Ndugai amemuelezea Mbunge Mstaafu wa jimbo la Kwela mkoani Rukwa Mzee Chrisant Mzindakaya kuwa alikuwa anapambana na rushwa kwa vitendo, na utumishi wake ndani ya Bunge umekuwa wa kutukuka.
https://www.youtube.com/watch?v=mrEnsRafgyw&feature=youtu.be
Akimtambulisha kwa Wabunge, Bungeni jijini Dodoma akiwa mgeni maalumu wa Spika, Ndugai amesema kuwa amemualika Mzee Mzindakaya ili Wabunge wengi waweze kujifunza kutokana na uzoefu wake wa miaka 45 ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akitolea mfano wa namna alivyoibua rushwa ndani ya Bunge, Spika Ndugai amesema kuwa, Mzindakaya aliibua rushwa ya Uagizwaji wa Sukari na kusababisha aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara katika serikali ya awamu ya Tatu, -Idd Simba kujiuzulu wadhifa wake.
Mzee Mzindakaya pia aliibua rushwa katika vibali vya uagizaji wa sukari nje ya nchi iliyomuhusisha Waziri wa Fedha wa wakati huo Profesa Simon Mbilinyi, kashfa iliyosababisha ajiuzulu wadhifa huo.
Katika serikali ya awamu ya Nne, Dkt Mzindakaya aliibua kashfa nyingine katika uuzwaji wa vitalu vya uwindaji iliyomuhusisha Waziri wa Maliasili na Utalii Shamsa Mwangunga, lakini hakufanikiwa kumuondoa katika wadhifa huo.
Dkt Mzindakaya pia ni Mjasiriamali anayemiliki kiwanda cha kuchakata nyama kilichopo mkoani Katavi na pia anamiliki Ranchi ya mifugo ambayo nayo ipo hukohuko Katavi.