Rais Mstaafu wa awamu ya Pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi ametoa wito kwa Serikali kushirikiana na Taasisi zisizo za Kiserikali, katika kukabiliana na matukio ya ukatili dhidi ya Watoto.
Alhaji Mwinyi ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati wa maadhimisho ya miaka 30 ya Siku ya Kimataifa ya Haki za Mtoto, maadhimisho yaliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF).
Amesema kuwa, ni muhimu kwa Wadau wote wanaoshughulika na masuala ya Watoto kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha haki za Watoto zinalindwa.
Rais huyo Mstaafu wa awamu ya Pili, pia amewataka Walezi pamoja na Wazazi nchini kuwa karibu na watoto wao, hatua itakayowawezesha kufahamu changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto hao.
