Mwili wa Dkt. Magufuli wasafirishwa kwenda Chato

0
475

Safari ya kuusafirisha mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli kuelekea nyumbani kwao Chato mkoani Geita imeanza ambapo mwili huo unasafirishwa kwa njia ya barabara ili kutoa nafasi kwa Wananchi wengi zaidi kuaga.

Safari hiyo imeanza baada ya mwili huo kumaliza kuzungushwa kwenye viunga vya jiji la Mwanza, ambapo maelfu ya Wananchi wamejitokeza njiani kupunga mkono wa kwaheri.

Ukiwa njiani msafara uliobeba mwili wa Dkt Magufuli utasimama kaika eneo la Busisi ambapo ni nyumbani kwa mjane wa marehemu, Mama Janeth Magufuli kwa ajili ya ibada ya dakika 10 kabla ya kuendelea na safari.

Wakazi wa Mwanza wanamkumbuka Dkt. Magufuli kwa mambo mengi aliyofanya na aliyokuwa akiendelea kufanya ikiwa ni pamoja na ukarabati wa uwanja wa ndege, ujenzi wa daraja la Kigogo-Busisi, upanuzi wa barabara za katikati ya mji, ujenzi wa daraja la waenda kwa miguu la Furahisha na uboreshaji wa huduma za afya na elimu.

Familia na wakazi wa Geita wataaga mwili huo Machi 25, 2021 kisha safari ya mwisho ya Dkt. magufuli hapa duniani itahitimishwa Machi 26, 2021 atakapolazwa kwenye nyumba yake ya milele.