Mwili wa Balozi Rupia waagwa Dar es Salaaam

0
438

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali inatambua mchango mkubwa uliotolewa na marehemu Balozi Paul Rupia wakati wa utumishi wake na hata baada ya kustaafu.

Amesema hayo alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika kuuaga mwili wa Balozi Paul Rupia katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam.

“Moja ya jambo ambalo halitasahaulika ni uthubutu wake wa kuanzisha Benki ya Watu wa Dar es Salaam (DCB) ambayo alikuwa mwenyekiti wake na hadi anaondoka katika uongozi aliiacha benki hiyo ikiwa na matawi manane na moja kati ya hayo likiwa jijini Dodoma,” amesema Majaliwa

Waziri Mkuu amewasihi Watanzania kumuombea marehemu na familia yake kwa Mwenyezi Mungu ili apate pumziko la milele na familia iwe na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema marehemu Balozi Rupia alichangia kwa kiasi kikubwa mageuzi ya uchumi nchini na kuanzisha mageuzi ya kisiasa ya mfumo wa vyama vingi.