Mwigulu: Thamani ya shilingi ya Tanzania ni tulivu

0
112

Wizara ya Fedha na Mipango imesema hadi kufikia Aprili 2023, thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya sarafu za nchi washirika wakuu wa kibiashara imeendelea kuwa tulivu licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali za kiuchumi duniani hususani ongezeko la bei za bidhaa.

Waziri wa wizara hiyo Dkt. Mwigulu Nchemba akiwasilisha taarifa ya Hali ya Uchumi kwa mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa mwaka 2023/2024 bungeni jijini Dodoma amesema, katika mwezi Aprili, 2023 Dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa shilingi 2,324.07 ikilinganishwa na shilingi 2,322.16 kipindi kama hicho mwaka 2022.

Aidha, katika kipindi cha kuanzia Aprili 2022 hadi Aprili 2023 Dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa shilingi 2,310.14.

Waziri Nchemba ametaja sababu za utulivu wa shilingi kuwa ni kutokana na utulivu wa mfumuko wa bei nchini ukilinganishwa na nchi washirika wa kibiashara, utekelezaji wa sera thabiti za fedha na bajeti, na uwepo wa chakula cha kutosha nchini Tanzania.