Mwenyekiti CCM Taifa akemea makundi

0
72

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wanachama wa chama hicho kutojenga nyufa ndani ya chama baada ya chaguzi kukamilika.

Dkt Samia ametoa kauli hiyo mkoani Dodoma wakati wa siku ya pili na ya mwisho ya mkutano mkuu wa 10 wa CCM.

Amesema ndani ya CCM bado kuna makundi ambayo yanaendeleza nongwa hata baada ya kumalizika kwa chaguzi hizo.

Dkt. Samia amesema makundi hayo hayajengi chama na badala yake yanakidhoofisha na kukifanya kushindwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Amesema anapenda kukiona Chama Cha Mapinduzi kikiendelea kuwa chama na chombo madhubuti cha kufuta unyonyaji wa aina zote na kupambana na jaribio lolote la uonevu.

Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa pia amekumbusha majukumu ya chama hicho kuwa ni pamoja na kuisimamia serikali ili iweze kuwaletea maendeleo wananchi wake.