Mwenyekiti CCM awataka wenye nia kujitathmini kabla ya kugombea

0
256

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Taifa – Dkt John Magufuli leo amekagua maandalizi ya kumbi za mikutano na vikao vya chama vinavyotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Rais DKT Magufuli akiwa ameongozana na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Philip Mangula na Katibu Mkuu wa CCM Dkt Bashiru Ally amekagua kumbi za Kituo cha Mikutano Dodoma ambako utafanyika Mkutano Mkuu wa CCM na pia amekagua jengo la Ofisi za Makao Makuu ya CCM.

Dkt Magufuli amewapongeza wajumbe wa Sekretarieti ya CCM na wasimamizi wa ukarabati uliofanyika katika majengo hayo ambayo yanatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 20 Juni, mwaka huu.

Rais Dkt Magufuli amesisitiza kuwa pamoja na kufanyika kwa mchakato
wa uchaguzi ndani ya chama, Uchaguzi Mkuu lazima utakuwepo na hivyo
amewataka wanachama wote wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kujitathmini na kujiridhisha kama wanatosha kugombea nafasi wanazoziomba.

Magufuli amewataka wana CCM kote nchini kutembea kifua mbele na kuyasema mambo yote ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa wananchi, badala ya kuacha jukumu hilo kwa viongozi wachache.