Mwenge wa Uhuru watembelea mradi wa maji Gezaulole

Miundombinu

0
166

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imesema Kisima cha Gezaulole kina uwezo wa kuzalisha lita 29,000 kwa saa na kinaweza kuhudumia wakazi wapatao 2500. Ambapo miundombinu mingine ni pamoja na matanki mawili yenye ujazo wa lita 90,000 na lita 60,000.

Mradi huu ulikuwa ukisimamiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni ambayo iliomba DAWASA kuufufua mradi huo ili kuweza kutoa huduma kwa wananchi.

Akisoma taarifa ya mradi huo kwa Kiongozi wa Mbio maalumu wa Uhuru Luteni Juosephine Mwambashi, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Jamii DAWASA, Neli Msuya amesema, maboresho ya mradi huo yaligharimu jumla ya shilingi milioni 154.

“Mradi huu ulianza kufanya kazi mwezi Novemba mwaka 2019 na kupitia mradi huu DAWASA iliweza kufungua rasmi ofisi za mkoa wa kihuduma wa Kigamboni ambapo mradi huu unahudumia mitaa miwili ambayo ni Kizani na Mbwamaji”- amesema Neli

Kupitia mradi huu, wakazi 2100 sawa na asilimia 85% ya walengwa wa Mradi huo wanapata maji safi na salama kutoka DAWASA huku taasisi zinazotoa huduma kwa jamii nazo zikinufaika na mradi huo.

Aidha amesema DAWASA waliamua kukarabati mradi huo uliojengwa na aliyekuwa Raisi wa Awamu ya Kwanza na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1970 kwa ajili ya kutoa huduma kwa kijiji cha ujamaa ili kuendelea kumuenzi Baba wa Taifa.

Naye Kiongozi wa Mbio Maalumu za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2021, Luteni Josephine Mwambashi amesema wananchi wanawajibu wa kulinda vyanzo hivyo vya maji pamoja na miundombinu ya maji ili kuweza kufikia hadhima ya kumtua mama ndoo kichwani.

Amesema Mwenge wa Uhuru mwaka 2021 umeamua kutembelea mradi huo ili kuona uwezo wake wa kuwahudumia wananchi wa mitaa miwili mara baada yakuzinduliwa mwaka 2019.