Mwenge wa Uhuru wasisitiza utunzaji wa mazingira

0
279

Utunzaji wa mazingira unapaswa kupewa kiupaumbele hasa kwenye vyanzo vya maji ili kuweza kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.

Hayo yamesemwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2021, Luteni Josephine Mwambashi alipotembelea utunzaji wa chanzo cha maji cha mto Kizinga na kupanda mti katika chanzo hicho kilichoanza mwaka 1950 ambacho kina uwezo wa kuzalisha maji kiasi cha lita milioni 7 hadi 9 kwa siku.

Amesema Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa kushirikiana na wananchi wanapaswa kuwa walinzi bora kwenye kulinda vyanzo vya maji, kwani vyanzo vikikauka hakutakuwa na haja ya kuwepo kwa mamlaka hiyo.

Ameongeza kuwa Mwenge wa Uhuru mwaka 2021 umetembelea chanzo hicho kuona uwezo wake wa uzalishaji wa maji pamoja na kuhamasisha upandaji wa miti kwenye vyanzo mbalimbali vya maji.

Akisoma taarifa ya utunzaji wa chanzo cha maji, Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji Maji kutoka (DAWASA), Mhandisi Shabani Mkwanywe amesema DAWASA kupitia mtambo wa mtoni iliweka lengo la kuongeza mtandao wa huduma ya maji ikiwemo kufikisha maji katika Tenki la Mbagala ili kuwafikia watumiaji wapya zaidi 100,000.

Utunzaji na upandaji wa miti katika chanzo hiki umesaidia kuongezeka kwa wingi wa maji ambayo kwa sasa yamewezesha kuwafikia watumiaji wapya 168,450 ambao hapo awali huduma ilikuwa haijawafikia. Amesema DAWASA itaendelea kutoa elimu kwa jamii inayokaa karibu na hifadhi ya mto ili kuhakikisha lengo la Serikali la kumtua mama ndoo ya maji kichwani linafikiwa.