Waziri wa TAMISEMI ameuagiza Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) kurejesha huduma ya usafiri wa mabasi ya mwendokasi kama kawaida kabla ya Juni Mosi mwaka huu ili kumaliza kero zinazowakabili wananchi.
Selemani Jafo amesema kuwa kwa siku za hivi karibuni kumekuwepo na msongamano mkubwa wa abiria kwenye vituo vya mabasi hayo kutokana na watu wengi kuanza kurejea kwenye shughuli zao mbalimbali kufuatia kupungua kwa ugonjwa wa corona.
“Ni kweli, baada ya Rais wetu, Dk John Pombe Magufuli kueleza matumaini makubwa ya idadi ya maambukizi kupungua nchini, watu wamerejea kwa kasi katika shughuli za kiuchumi, hii imechangia msongamano pale Kimara nyakati za asubuhi hasa tukikumbuka pia kuwa ni ‘level seat’,” amesema Jafo akizungumza na gazeti la Habarileo.
Jafo amesema kuwa wasimamizi wa mradi huo wamemueleza kuwa mbali na idadi ya watu kuongezeka, lakini idadi ya magari yanayotoa hudumu nayo imepungua, kwani mabasi marefu 30 yapo katika matengenezo.
Aidha, ameagiza magari hayo kufanyiwa matengenezo haraka, kwani kutokana na maisha kuanza kurudi katika hali kawaida, na vyuo kufunguliwa, usafiri huo utahitajika sana kuhakikisha watu wanawahi kwenye shughuli zao.