Mwalimu Nyerere na juhudi binafsi darasani

0
205

Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipata elimu yake ya msingi katika shule ya Mwisenge iliyopo Musoma mkoani Mara kati ya mwaka 1934 na 1936.

Kwa yeyote anayefika shuleni hapo lazima atasikia sifa zinazomuelezea Julius Nyerere alikuwa ni mwanafunzi wa aina gani, zaidi ni kuwa alikuwa mwenye juhudi binafsi katika kujifunza.

Hali hiyo ilimsaidia sana kufanya vizuri kwenye masomo yake darasani na pia kwenye mitihani yake mbalimbali.

Mwalimu Mkuu wa sasa wa shule ya msingi Mwisenge, Thomas Sigawa anasema miongoni mwa sifa alizojizolea Julius Nyerere akiwa mwanafunzi wa shule hiyo ni ile ya kuwa na uwezo mkubwa darasani tofauti na wenzake.

Ametolea mfano akiwa darasa la pili, Julius alifaulu kwa alama za juu na kuwapita Wanafunzi wenzake wote ukanda wa Afrika Mashariki, na hivyo kufanya kurushwa darasa kutoka la pili kwenda la nne.

Hakuishia hapo, Mwalimu Sigawa anasema alipokuwa darasa la nne Julius Nyerere aliendelea kuonesha utofauti wake na Wanafunzi wengine na hapo ndipo alipopata ufaulu wa juu zaidi na kuwazidi wenzake wa Tanganyika na kuchaguliwa kwenda kuendelea na masomo ya sekondari mkoani Tabora katika shule ya sekondari ya Wavulana Tabora .

Sifa nyingine ya Julius Nyerere ni kwamba alikua Mwanafunzi aliyependa hali ya utulivu, na ndio maana wakati wa muda wake wa ziada alibeba dawati lake na kukaa peke yake chini ya mti nje ya shule hiyo ili kujisomea kwa utulivu.

Kila siku, akiwa Mwanafunzi wa shule hiyo Julius Nyerere alitembea umbali wa takribani kilomita 60 kutoka Mwitongo wilayani Butiama hadi Mwisenge wilayani Musoma kwenda shuleni na kurudi nyumbani akiwa darasa la kwanza na la pili mpaka alipopata nafasi ya bweni akiwa darasa la nne.

Katika kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, uongozi wa shule ya msingi Mwisenge umeweka kumbukumbu ya dawati eneo palipokuwa na mti, mahali ambapo Baba wa Taifa akiwa Mwanafunzi shuleni hapo alitumia muda wake wa ziada kwa ajili ya kujisomea.