Mwalimu Nyerere alichukia neno njaa

0
161

Wakati wa uhai wake, Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alithamini sana shughuli za kilimo kilichoajiri asilimia 65 ya Watanzania na kuchangia asilimia 27 katika pato la Taifa.

Licha ya hadhi na madaraka aliyokuwa nayo, Mwalimu Nyerere aliheshimu sana kazi za kilimo akiamini kuwa kilimo ndio uti wa mgongo wa Taifa la Tanzania.

Madaraka Nyerere ni mmoja wa watoto wa Hayati Baba wa Taifa, na anasema baba yake alichukizwa sana na neno njaa na ndio maana hata wakati wa mapumziko yake kijijini Butiama, Musoma mkoani Mara alitumia muda wake mwingi kushinda shambani kufanya shughuli za kilimo na ufugaji hadi siku za mwisho za uhai wake.

Madaraka amesema walipokua wakienda kijijini Butiama wakati wa likizo mwisho wa mwaka, Marehemu Baba yao alikua akitumia muda mwingi shambani kulima, aliamini ndio njia sahihi ya kukabiliana na njaa ndani ya familia yake na alikua akiwahamasisha wageni na Wananchi waliokuwa wakimtembelea kushiriki katika shughuli za kilimo.

“Ilikuwa tukija Butiama wakati wa likizo na hata alipostaafu kazi za Serikali Mwalimu alitumia muda mwingi kuwa shambani, hata leo hii nje ya nyumba aliyojengewa na Chama cha TANU kuna vihenge, sehemu maalum za kuhifadhia ulezi na mazao mengine.” ameongeza Madaraka Nyerere

Kisiri Jackton Nyerere ni miongoni mwa Wanafamilia ya Hayati Baba wa Taifa na kumbukumbu zake ni kuwa
hata Viongozi mbalimbali waliokwenda kumuona Mwalimu Nyerere kijijini Butiama iliwabidi wamfuate shambani na mazungumzo yalikua yakifanyika huku wakiendelea na kilimo.

Kingine anachokumbuka Kisiri Jackton Nyerere ni siku moja walipokua shambani pamoja na Mwalimu Nyerere mvua kubwa ilinyesha na kusababisha gari yao kukwama hali iliyowalazimu kufanya juhudi za kulikwamua hadi saa nne usiku wakiwa na Mwalimu.

“Alipenda kushirikiana na sisi kwa kila kitu, siku moja mvua kubwa ilinyesha tukiwa bado shambani na Mwalimu akasema tuendelee na kazi hadi giza linaingia bado tupo shambani, lakini wakati wa kurudi gari ikanasa kwenye matope, wakati tunafanya juhudi za kulitoa topeni Mwalimu naye alikuja kutusaidia kusukuma gari hakujali cheo alichonacho.” ameongeza Jackson.