Watu 24 wamekufa na wengine wengi wamejeruhiwa baada ya mvua kubwa kunyesha kwenye jimbo la Cibitoke nchini Burundi.
Habari kutoka nchini Burundi zinaeleza kuwa, jitihada za uokoaji zinaendelea baada ya nyumba nyingi katika jimbo hilo kusombwa na maporomoko ya udongo pamoja na mafuriko yaliyosababishwa na mvua hizo.
Wafanyakazi wa uokoaji wanaendelea kufukua matope ili kuona kama wanaweza kupata miili ya watu waliokufa.
Jimbo hilo la Cibitoke ambalo ni la milima mingi, limekua likipata mvua nyingi ambazo zimekua pia zikisababisha maporomoko ya udongo na mafuriko.
Mvua kama hizo pia zimenyesha kwenye nchi za Kenya na Uganda na kusababisha maporomoko ya udongo na mafuriko, na mpaka sasa takribani watu 130 wamefariki Dunia katika nchi hizo.