Muhimbili yafunga mashine za mamilioni Hospitali ya Amana

0
637

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imefunga mashine tatu za kusafisha damu kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo zenye thamani ya TZS. milioni 210 na inatarajia kufunga mashine moja ya kusaidia mgonjwa kupumua (ventilator) yenye thamani ya TZS. milioni 56 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana ili kuhudumia wagonjwa waliopata maambukizi ya virusi vya Corona.
 
Tayari wagonjwa wanaohitaji kusafishwa damu wameanza kuhudumiwa ambapo dawa na vitendanishi vya kutoa huduma ya kusafisha figo kwa sasa vinagharimiwa na muhimbili.
 
Sambamba na hilo, hospitali imefunga mtambo wa kuchuja maji (Portable RO) wenye thamani ya TZS milioni 28 na mtandao wenye miundombinu ya kusafirisha maji ili kuwezesha mashine hizo kufanya kazi ya kusafisha damu uliogharimu TZS milioni 12.

Kutokanana hilo, MNH itapokea madaktari na wauguzi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Amana kuanzia tarehe Aprili 28, 2020 ili kujengewa uwezo kwenye Kitengo cha Kusafisha Damu pamoja na vyumba vya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICUs) aina tano tofauti.
 
Aidha, MNH imepokea wagonjwa 93 kutoka Amana wakiwemo watoto wachanga 30 chini ya mwezi mmoja wakiwa na mama zao, watoto wanne chini ya miaka mitano, kina mama wajawazito 36, wagonjwa wa upasuaji 10 na wagonjwa 13 wenye magonjwa ya ndani (internal medicine).
 
MNH imekua bega kwa bega na uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwenye maandalizi ya kupokea wagonjwa waliopata maambukizi ya Corona katika Hospitali Rufaa ya Amana ikiwa ni hatua ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha wagonjwa waliolazwa wanapata huduma.

MNH inatoa rai kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ili kujinga na kuwakinga wengine kulingana na maelekezo yanayotolewa na serikali.