Muhas yapata mashine ya kisasa ya kinywa na meno

0
404


Kupatikana kwa mashine kubwa ya kisasa katika Chuo Kikuu cha afya na sayansi shirikishi, Muhimbili(MUHAS), Skuli ya kinywa na meno kunaelezwa kuwa suluhisho kwa wagonjwa kusubiri muda mrefu kwa ajili ya uchunguzi wa kinywa na meno.

Hayo yamebainishwa mkoani Dar es Salaam na Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi, Muhimbili (MUHAS) Profesa Appolinary Kamuhabwa mara baada ya kupokea mashine hiyo iliyotolewa na timu wataalamu kutoka nchini Uturuki ikiongozwa na Balozi wa nchi hiyo nchini Dkt. Mehmet Gulluoglu.

Profesa Appolinary amesema uhusiano mzuri uliopo kati Tanzania na Uturuki umewezesha kupatikana kwa mashine hiyo ya kisasa yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 200 ambayo ni msaada mkubwa kwenye kitengo cha afya ya kinywa na meno na upande wa Skuli ya kinywa na meno.

Naye Balozi wa Ururuki nchini Dkt. Mehmet Gulluoglu ameahidi nchi hiyo kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika kuimarisha sekta ya afya nchini.

Nao baadhi ya wanafunzi wa Skuli ya Kinywa na Meno Muhimbili wamesema mashine hiyo ni msaada kwao katika kujifunza na kufanya tafiti mbalimbali za magonjwa ya kinywa na meno.