Mtendaji Mkuu wa Pride Tanzania atakiwa kujisalimisha

0
2103

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa  Nchini (TAKUKURU) imemtaka aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa taasisi iliyokuwa ikijishughulisha na utoaji mikopo ya Pride Tanzania, – Rashid Malima kujisalimisha kufuatia tuhuma za ubadhilifu wa shilingi bilioni moja nukta nane ambazo ni fedha za taasisi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Brigedia Jenerali John Mbungo amesema kuwa Malima amekimbilia nchini Marekani na kuwaomba watanzania wanaoishi nchini humo na wenye taarifa kamili kuhusiana na mtu huyo waziwasilishe katika taasisi hiyo.

Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Mbungo, TAKUKURU pia inamtafuta Josephat Machiwa aliyekuwa afisa mikopo wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Kitivo cha Elimu (DUCE) kwa madai ya kukimbia na fedha za ada za wanafunzi wa chuo hicho.

Katika hatua nyingine Brigedia Jenerali Mbungo amesema kuwa TAKUKURU imewakamata wafanyabiashara kadhaa katika eneo la  Kariakoo jijini Dar es salaam ambao wamekuwa wakiibia serikali kwa kutoa risiti za kielektroniki ambazo hazilingani na thamani ya fedha za manunuzi.

Amewakumbusha Watanzania wote kuwa kitendo chochote cha kutumia nyaraka zenye lengo la kuidanganya serikali kinahesabiwa kama rushwa chini ya kifungu cha 22 cha sheria ya TAKUKURU na hivyo kuwataka kutokubali kupokea risiti ambayo haiendani na thamani ya fedha za manunuzi ya bidhaa.