Mtendaji Mkuu TBA matatani, atakiwa kujitathmini

0
183

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemtaka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Daud Kondoro ajitathmini kuhusu utendaji kazi wake, huku akiwasimamisha kazi Wakurugenzi Watatu wa wakala huo.

Waziri Mkuu amewasimamisha kazi Wakurugenzi hao hii leo alipotembelea mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) eneo la Njedengwa jijini Dodoma.

Wakurugenzi waliosimamishwa kazi ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ujenzi, – Humphrey Killo, Kaimu Meneja wa Miradi Abdallah Awadh na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ushauri Hamis Kileo.

“TBA tunaihitaji lakini watu wake wana shida, hatuwezi kuwaacha, TBA wasipewe miradi kwa sababu hawawajibiki na wanadhani kwa kuwa ni Taasisi ya Serikali ndio wataachwa wafanye mambo ya hovyo”, amesema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu Majaliwa amechukua hatua hiyo baada ya kutoridhishwa na utendaji kazi wa TBA katika miradi mbalimbali waliyopewa na Serikali ukiwemo wa ujenzi wa jengo la NEC, ambalo ujenzi wake ulianza mwezi Julai mwaka 2017 na ulitakiwa ukamilike mwezi Juni mwaka 2018 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 13, lakini haujakamilika hadi sasa na umesimama.

Akiwa katika eneo hilo la mradi wa ujenzi wa ofisi ya NEC, Waziri Mkuu amehoji sababu za mradi huo kutokamilika kwa wakati, ambapo Kaimu Mkurugenzi wa Ujenzi alisema kuwa, jengo hilo limeshindwa kukamilika kwa sababu wakati walipokuwa wanaanza kazi walibaini kuwa kuna vitu vilisahaulika wakati wa uandaaji wa  BOQ.

 “Bajeti ya awali ilikuwa Shilingi Bilioni Kumi, wakati wa uandaaji wa michoro ya ujenzi gharama ziliongezeka na kufikia Shilingi Bilioni 13 ambazo ndizo tulikubaliana katika mkataba, wakati tunaendelea na kazi tuligundua kuna vitu vimesahaulika kwenye BOQ, jambo lililoongeza bajeti ya ujenzi na kufikia Shilingi Bilioni 32”, alisema  Killo.

Waziri Mkuu Majaliwa ameongeza kuwa, miradi mingi inayojengwa na TBA katika maeneo mbalimbali nchini imeshindwa kukamilika kwa wakati, hivyo amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Jenista Mhagama asitishe mkataba huo wa ujenzi na atafutwe mkandarasi mwingine ili amalizie.

 “Jengo la TAMISEMI lililopo katika mji wa Serikali limejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 1.7, nyie wataalamu gani na kwa nini tuendelee kuwaacha ndani ya Taasisi?, TBA hamfanyi kazi vizuri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanalalamika majengo hayakamiliki, ni Serikali gani itakayowavumilia, mmeshindwa kutambua majukumu yenu”, amehoji Waziri Mkuu Majaliwa.