Mtatiro afanya ukarabati mkubwa uwanja wa CCM Tunduru

0
170

Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro, ameanza harakati za kuufufua uwanja wa CCM Tunduru.

Taarifa kutoka Tunduru zimeeleza kuwa uwanja huo unakarabatiwa katika kiwanja cha kuchezea (pitch) kwa kumwaga na kushindilia ‘trip’ 200 za kifusi, kisha zitawekwa ‘trip’ 56 za udongo wenye rutuba na kisha kupandwa nyasi wakati huu wa mvua.

Kazi nyingine zitakazofanyika ni pamoja na kununua mashine za kisasa za kutunza uwanja, kufunga taa, kukamilisha uzio wa ndani, mitaro ya kutolea maji, kuweka mageti mapya na vifaa vya kukinga ukuta mkuu usivamiwe na watu kukaa juu.

DC Mtatiro amesema imemchukua miaka miwili kupanga mikakati inayozaa matunda makubwa na kwamba kazi zote zitakapokamilika zitagharimu shilingi milioni 120 zinazotokana na michango ya hiari ya watu na taasisi mbalimbali.

Mtatiro amesema kazi kuu ya serikali ni kuweka miundombinu yote muhimu ili wananchi waitumie kujiletea maendeleo na kutaja kuwa michezo ni kati ya sekta inayobeba mamilioni ya vijana, kwahiyo Tunduru inaichukulia sekta hiyo kwa uzito kama ilivyo kwa shughuli nyingine za maendeleo.

Amewashukuru sana wadau wote wa maendeleo wilayani Tunduru ambao wanaiunga mkono serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika nyanja zote ikiwemo michezo.