Mwili wa Mtanzania Nemes Tarimo (37) aliyefariki dunia katika vita kati ya Russia na Ukraine umewasili nchini hii leo ambapo unaagwa mkoani Dar es Salaam, kabla ya kusafirishwa kwenda mkoani Mbeya kwa ajili ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika hapo kesho.
Mapema hii leo katika uwanja wa ndege wa kimataifa ya Julius Nyerere mkoani Dar es Salaam, mwili wa Nemes umepokelewa na ndugu, jamaa na marafiki.
Nemes alikwenda Russia miaka kadhaa iliyopita kwa ajili ya masomo, lakini hata hivyo mwaka 2021 alipatikana na makosa yanayohusiana na dawa za kulevya na kuhukumiwa kifungo cha miaka saba jela.
Mwaka 2022 akiwa anaendelea kutumia kifungo chake alisaini mkataba na jeshi la kukodi la Russia, Wagner ili aende kupigana vita vinavyoendelea kati ya Russia na Ukraine ambapo pindi vita hiyo ingemalizika angeachiwa huru.