Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini kufanya uchunguzi kwenye vyama mbalimbali vya siasa ili kujiridhisha endapo vilifuata Kanuni na Sheria hadi ulipofika mchakato wa
uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Akizungumza na Waandishi wa habari katika Ofisi ndogo za CCM zilizopo Lumumba jijini Dar es salaam, –
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM,- Humphrey Polepole amedai kuwa, kuna taarifa kwamba baadhi ya vyama hivyo vya siasa havikuwa na
mchakato wa uteuzi wa Wagombea, hatua ambayo ni ukiukwaji wa Kanuni na Sheria za vyama vya siasa
Amesisitiza kuwa, tofauti na vyama vingine CCM iliwekeza katika kuelimisha Wanachama wake juu ya uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa na ilipeleka Wanasheria katika wilaya zote nchini ili kuwasaidia Wagombea katika ujazaji fomu na kuzingatia kanuni
tofauti na vyama vingine.
CCM imesema kuwa mpaka sasa mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa umeenda vizuri na kuitaka Serikali kuendelea kuwa imara na kutoyumbishwa na
malalamiko ya baadhi ya vyama vya upinzani ambavyo Wagombea wao
walienguliwa kwa kutokidhi matakwa ya kisheria.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa umekuwa ukifanyika mwaka mmoja kabla ya Uchaguzi Mkuu na kwa mwaka huu utafanyika Novemba 24.
