Mradi wa maji Mkuranga wawekewa jiwe la msingi

0
240

Mbio za Mwenge wa Uhuru, zimeweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maji Mkuranga – Vikindu kwa lengo la kuwezesha wananchi wa Mkuranga na kata zake kuendelea kupata huduma ya maji safi.

Akiongea wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi kwenye mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Sahili Geraruma, amesema ameridhika na utekelezaji wa mradi huo na kwamba utanufaisha wakazi wengi wa Mkuranga na maeneo ya jirani.

“Nimekagua kazi zote zilizofanyika kwenye mradi ikiwemo ujenzi wa chanzo cha kuzalisha maji chenye uwezo wa kuzalisha lita 284,400 kwa saa, pamoja na tenki la kuhifadhi maji Mkuranga lenye ujazo wa milioni 1.5.

“Rais Samia Suluhu Hassan anawapenda wakazi wa Mkuranga na ndio maana amewezesha mradi huu kutekelezwa kwa kasi ili kumtua Mama ndoo ya maji kichwani,”-amesema Geraruma.

Amesema kuwa hii ni sehemu ya nia njema ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyonayo ya kuhakikisha wananchi wote wanapata maji safi ipasavyo. Ameitaka DAWASA kuhakikisha huduma ya maji inakua endelevu na wananchi wanapata majisafi muda wote.

Akitoa maelezo ya utekelezaji wa mradi Mkurugenzi wa Miradi DAWASA, Mhandisi Ramadhani Mtindasi amesema kuwa mradi wa Mkuranga umetekelezwa kwa fedha za ndani za Mamlaka kiasi cha shilingi bilioni 5.5 kwa kutumia chanzo cha maji chenye kina cha mita 545 ambacho kinauwezo wa kuzalisha maji lita 284,400 kwa saa.