Mradi wa maji Mkuranga wakamilika

0
158

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeiagiza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuhakikisha inafikisha huduma ya maji kwa Wakazi wa Vikindu hadi Kongowe baada ya kukamilika kwa mradi wa maji Mkuranga uliopo Mkuranga mkoani Pwani. 
 
Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea mradi wa maji Mkuranga, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Japhet Hasunga amesema,  mradi wa maji Mkuranga umetekelezwa kwa ufanisi mkubwa na kamati imeridhika na kazi iliyofanyika.  
 
“Tumetembelea mradi na tumeona kazi iliyofanyika, tumeridhika kusikia kuwa Wananchi wanapata maji kutoka kwenye chanzo hiki,” amesema Hasunga  
 
Amesema wakati umefika kwa Menejimenti ya DAWASA kujenga tenki lingine la kufikisha maji kwa wakazi wa Mwanambaya, Vikindu mpaka Kongowe ili wakazi wa maeneo hayo wapate maji.
 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya DAWASA, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Mstaafu Jenerali Davis Mwamunyange amesema, bodi hiyo  imepokea maagizo yote kutoka kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali na kazi itaenda kutekelezwa ili kuhakikisha Wananchi walengwa wanapata  huduma ya maji..
 
“Tutajitahidi sana kutekeleza maagizo yote ya kamati yaliyotolewa ili huduma ya maji safi ipatikane kwa Wakazi wote kwa maeneo yaliyoainishwa na Kamati” amesema Jenerali Mstaafu Mwamunyange. 
 
Mradi wa maji Mkuranga umetekelezwa na DAWASA kwa gharama ya shilingi bilioni 5.5  kwa kutumia chanzo cha maji ambacho ni kisima cha maji chenye kina cha mita 545 chenye uwezo wa kutoa zaidi  ya lita laki mbili na themanini elfu kwa saa.
 
Mradi huo umekamilika kwa asilimia mia moja na unahudumia Wakazi  wa kata za Kiparag’anda katika mitaa ya Mkuranga A, Mkuranga B, Kiguza, Mgawa, Bigwa, Mkwalia – Kitumbo, Njia nne na  Sunguvuni huku wateja 2,154 wakiwa wameunganishiwa huduma ya maji kupitia mradi huo.