MO awashukuru Watanzania kwa maombi

0
2280

Msemaji wa familia ya mfanyabiashara maarufu nchini Mohamed Dewji maarufu kama MO aliyetekwa hivi karibuni, -Azim Dewji amesema kuwa baadae hii leo watazungumza na waandishi wa habari kuhusu kupatikana kwa mfanyabiashara huyo.

Azim amesema kuwa MO aliachiliwa na watekaji hao majira ya saa nane usiku kuamkia hii leo, ambapo watekaji hao walimuacha katika viwanja vya Gymkana vilivyopo jijini Dar es salaam akiwa salama.

Mo mwenyewe amemweleza Kamanda wa Polisi Kanda maalum ya Dar es salaam,- Lazaro Mambosasa kuwa yuko salama na anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuungana na familia yake.

Ameishukuru serikali na vyombo vyote vya ulinzi na usalama kwa jitihada kubwa za kumtafuta katika kipindi chote na pia amewashukuru watanzania wote kwa dua na maombi yao.

MO alitekwa Oktoba 11 mwaka huu na watu wasiofahamika katika hoteli ya Collessium iliyopo jijini Dar es salaam alikokwenda kufanya mazoezi.