Mkuu Mpya JKT

0
228

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan amemteua Brigedia Jenerali Rajabu Mabele kuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Uteuzi huo umeanza Mei 19, 2021 kufuatia kuteuliwa kwa aliyekuwa Mkuu wa Jeshi hilo, Meja Jenerali Charles Mbuge kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.

Brigedia Jenerali Mabele alijiunga na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Novemba 25, 1993 na kutunukiwa Kamisheni kuwa Afisa Machi 25, 1995.

Pamoja na taaluma nyingine za Kijeshi, Brigedia Jenerali Mabele ana Shahada ya Uzamili katika Usimamizi wa Biashara (Masters of Business Administration) ambapo alijikita katika Usimamizi wa Mashirika (Corporate Management).

Sambamba na uteuzi huo, Rais na Amiri Jeshi Mkuu Samia Suluhu Hassan amemteua Kanali Absolomon Shausi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa SUMA-JKT.

Kabla ya uteuzi huo Kanali Shausi alikuwa Naibu Mkurugenzi wa shirika hilo.