Mkurugenzi wa Fedha DART asimamishwa kazi

0
144

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Fedha na Maendeleo ya Biashara wa Wakala wa Mabasi yaendayo haraka nchini (DART) Suzana Chaula, huku akiweka wazi kuwa tatizo lililopo kwenye mradi huo si uwezo bali ni usimamizi mbovu.

Waziri Mkuu Majaliwa amefikia uamuzi huo hii leo wakati wa ziara yake katika baadhi ya vituo vya mabasi yaendayo haraka mkoani Dar es salaam, ambapo pia amebaini utendaji kazi na ufuatiliaji mbovu katika mradi huo.

“Tunataka tujenge mradi awamu ya tatu kwenda Gongo la Mboto, na tunajenga awamu hii kwa kukusanya fedha kununua mabasi kwa ajili ya awamu nyingine uwezo huo upo, hatuwezi kuvumilia msimamizi ambaye hawezi akiwemo Mkurugenzi wa fedha, Hii fedha sisi tumekopa World Bank na tunalipa fedha yetu ya ndani ya walipa kodi wa Tanzania, leo tunaweka watu hawafanyi kazi vizuri,”amesema Waziri Mkuu.

Amesema mfumo unaotumika wa uuzaji wa tiketi ni mbovu, na unaikosesha Serikali mapato mengi jambo.ambalo halikubaliki.

“Mtu anauza tiketi zake ndipo auze za Serikali na Watendaji wapo, wanaona na hawachukui hatua, leo nimewauliza tangu Mkurugenzi Mkuu ameingia DART ana miaka mitano amenunua mabasi mangapi hakuna hata moja, anasema hana fedha,” ameongeza Waziri Mkuu Majaliwa.