Mkurugenzi sikuondoi, chapa kazi : kauli ya Rais Magufuli

0
286

Rais John Magufuli amesema kuwa, hatamuondoa katika wadhifa huo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ileje mkoani Songwe,- Haji Mnasi kwa kuwa taarifa ilizonazo mpaka sasa ni kwamba hana tuhuma zinazosababisha aondolewe katika nafasi hiyo.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo wilayani Ileje wakati akizungumza na Wakazi wa wilaya hiyo ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya siku Nne mkoani Songwe.

Rais Magufuli amelazimika kutoa kauli hiyo baada ya Mbunge wa jimbo la Ileje, – Janeth Mbene kumueleza Rais Magufuli wakati wa mkutano huo kuwa, Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Halmashauri amekua akikwamisha shughuli nyingi za maendeleo ya wilaya ya Ileje.

Amesema kuwa, atafanya uchunguzi kwa kutumia vyombo vyake ili kuona kama ana tuhuma, kwa kuwa mpaka sasa taarifa ilizonazo ni kuwa Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Halmashauri ya wilaya ya Ileje anapenda kufundisha na mara nyingi amekua akiingia darasani kufundisha.

“Taarifa niliyonayo hata waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo ni shahidi, huyu Mkurugenzi siku nyingine hafanyi kazi zake anakwenda kufundisha darasani, sasa Mkurugenzi simtoi hadi nipate information zangu mwenyewe, wakati mwingine taarifa zinakuja kuwa anashiriki kwenye siasa, kama unatafuta ubunge nitajua, tuache kuchongea watu, uongozi ni pamoja na kuvumiliana, lakini kama anakwenda kufundisha ndio vizuri si anawafundisha watoto wenu”, amesema Rais Magufuli.