Mkonge kuipaisha Tanzania kiuchumi

0
185

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha zao la mkonge linaendelezwa na kuwanufaisha watu wote wanaoshughulika na zao hilo.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo mkoani Tanga wakati wa mkutano ulioshirikisha Wadau mbalimbali wa zao la mkonge, mkutano ambao pia utapokea taarifa kuhusu utekelezaji wa mambo mbalimbali kuhusu uendelezaji wa zao la mkonge.

Amesema kwa sasa uhamasishaji unaendelea ili watu wengi zaidi wajishughulishe na kilimo cha mkonge na kwa kufuata ushauri wa Wataalam wa kilimo.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali itahakikisha zao la mkonge linatoa mchango wake katika kukuza uchumi wa Taifa na kuwaongezea kipato Wakulima wa zao wa hilo.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, Serikali inaendelea kufanya jitihada kubwa kuhakikisha zao la Mkonge linalimwa kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, ambapo lilikuwa likilimwa katika maeneo.mbalimbali hapa nchini.

Jitihada hizo ni pamoja na kuifufua Bodi ya Mkonge Nchini, hatua ambayo itasaidia kuendelezwa kwa zao la mkonge.

Waziri Mkuu Majaljwa pia amewashauri Wakulima wa zao la mkonge katika maeneo mbalimbali nchini kuunda ushirika, ambao utawasaidia katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata mikopo itakayowawezesha kukuza kilimo hicho.