Mkoa wa Iringa wafanya mapinduzi katika uwekezaji

0
253

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo anatarajiwa kuzindua mwongozo wa uwekezaji mkoa wa Iringa ikiwa ni mkakati wa mkoa huo kuonesha fursa za uwekezaji zilizopo na kuvutia wawekezaji.

Akizungumza kupitia kipindi cha Jambo Tanzania ndani ya TBC1, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi amesema uzinduzi huo utahusisha kuzinduliwa kwa kitabu (nakala ngumu) pamona na tovuti, vyote vyenye taarifa muhimu za uwekezaji.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi akisoma kitabu cha Mwongozo wa Uwekezaji Mkoa wa Iringa ambacho kitazinduliwa leo na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Hafla ya uzinduzi huo inafanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa.

Hapi amesema kuwa, muwekezaji yeyote yule cha kwanza anachokitaka kabla ya kuwekeza ni taarifa, na hivyo muongozo huo utaeleza kiundani maeneo ya uwekezaji yaliyopo Iringa, uwekezaji unaoweza kufanyika, hivyo wawekezaji hawatakuwa na haja ya kuwa na timu za tafiti.

Amesema lengo la kuzindua tovuti ni ili kuweza kuhuisha taarifa za uwekezaji kila baada ya miezi mitatu, hivyo kufanya taarifa kwenda na wakati.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi akizungumza hafla ya uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji

Aidha, ameongeza kuwa, mbali na kueleza fursa za uwekezaji, mwongozo huo unaeleza namna ya kupambana na vitendo vya rushwa na vitendo vingine vinavyodhorotesha uwekezaji mkoani Iringa.

Mbali na Waziri Mkuu kuzindua mwongozo huo, wananchi watapata fursa ya kutembelea mabanda ya wawekezaji na kujionea bidhaa na huduma mbalimbali na pia Waziri wa Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo atazungumza na wawekezaji hao.