Mke wa Waziri Mkuu wa Lesotho anatarajiwa kushtakiwa kwa kosa la kuhusika na mauaji ya mke wa kwanza wa kiongozi huyo yaliyotendeka mwaka 2017, polisi wameeleza.
Maesiah Thabane, ambaye alitoroka nchini humo Januari 10 mwaka huu na kukimbilia Afrika Kusini kuepuka kukamatwa, alirudi nchini humo na kujisalimisha katika kituo cha polisi kilichopo katika mji mkuu wa nchi huyo, Maseru.
Kaimu Kamishna wa Polisi, Mokete Paseka amesema kuwa mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani mara mkurugenzi wa mashtaka atakapokamilisha uandaaji wa hati ya mashtaka.
Hati ya kukamatwa kwa Thabane ilitolewa baada ya mwanamama huyo kutokuripoti polisi kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na mauaji ya Lipolelo Thabane.
Mauaji hayo yalitokea siku mbili kabla Waziri Mkuu, Thomas Thabane hajaapishwa kwa ajili ya muhula wa pili, na miaka miwili baada ya mahakama kuamuru kuwa Lipolelo ndiye mke halali (first lady) na anastahili sehemu ya mali (benefits).
Mke huyo mpya aliolewa miezi miwili baada ya mauaji hayo kutokea, ambapo wawili hao wanatuhumiwa kuhusika na kifo hicho, na tayari waziri huyo alishahojiwa ikidaiwa kuwa alitumia simu yake kuwasiliana na aliyekuwa eneo la tukio.
Waziri mkuu huyo mwenye miaka 80, mwezi uliopita alitangaza kuwa atajiuzulu baada ya chama chake kumtaka kufanya hivyo. Hata hivyo hakubainisha kwamba ni lini atajiuzulu, ila alisema atafanya hivyo mambo yote yakiwa tayari.