Mkandarasi anayejenga daraja la Kigongo – Busisi atakiwa kuongeza kasi

0
228

Rais Dkt John Magufuli amekagua maendeleo ya ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi ambalo litakuwa na urefu wa Kilometa 3.2, na hivyo kuwa daraja refu kuliko yote Afrika Mashariki na Kati.

Daraja hilo ambalo linajengwa na Mkandarasi China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) kwa gharama ya takribani Shilingi Bilioni 700, linatarajiwa kukamilika mwezi Februari mwaka 2024.

Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Mwanza, – Mhandisi Vedastus Maribe amesema ujenzi wa daraja hilo ulioanza Februari 25 mwaka huu umefikia asilimia 11.18 ikiwemo ujenzi wa daraja la muda ambao umefikia asilimia 51.6 na kwamba hadi kukamilika kwake linatarajiwa kuwa na nguzo 67 zikiwemo tatu kubwa.

Akizungumza baada ya kujionea kazi ya uchimbaji wa mashimo yenye urefu wa Meta tatu ndani ya mwamba kwa ajili ya ujenzi wa nguzo hizo, Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa na hatua iliyofikiwa, lakini amemtaka Mkandarasi CCECC kuongeza kasi ya ujenzi kwa kufanya kazi usiku na mchana ili likamilike haraka na kuanza kutumika.

Rais Magufuli amesema daraja hilo lina umuhimu mkubwa kwa Watanzania na nchi jirani za Uganda, Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Amewapongeza wananchi wa Kanda ya Ziwa kwa kujengwa kwa daraja hilo ambalo litaepusha ajali za mara kwa mara za kuzama kwa mitumbwi inayovusha watu na bidhaa mbalimbali kati ya Kigongo na Busisi.

Ametoa wito kwa Wananchi hasa vijana wanaopata ajira katika mradi huo, kufanya kazi kwa bidii na uadilifu badala ya kuiba vifaa vya ujenzi.

Tayari Rais Magufuli amewasili nyumbani kwake Chato mkoani Geita.