Mkakati wa nne wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi wazinduliwa

0
1706

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua Mkakati wa Nne wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi wa mwaka 2018/2019 hadi mwaka 2022/2023, unaotarajiwa kupunguza maambukizi mapya ya Virusi vinavyosababisha Ukimwi kwa asilimia 75 ifikapo mwaka 2020 na asilimia 85 ifikapo mwaka 2023.

Matokeo mengine yanayotarajiwa kufikiwa kutokana na mkakati huo ni kupungua kwa maambukizi mapya ya Virusi vinavyosababisha Ukimwi miongoni mwa watoto kwa chini ya asilimia tano ifikapo mwaka 2023 na chini ya asilimia 2 ifikapo mwaka 2030.

Waziri Mkuu Majaliwa amezindua mkakati huo kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika Kitaifa jijini Dodoma na kuongeza kuwa matayarisho ya mkakati huo yamezingatia matokeo ya mapitio ya Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi wa mwaka 2013/2014 hadi 2017/2018.

Amesema kuwa mbali na matokeo hayo, mkakati huo pia utawezesha kupungua kwa vifo vinavyohusiana na ukimwi kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2020 na asilimia 70 ifikapo mwaka 2023 na kupunguza unyanyapaa ifikapo mwaka 2023 na kuelekea kutokomeza kabisa ifikapo mwaka 2030.

Hata hivyo Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa mkakati huo wa Nne wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi umewianisha na kupanga programu mbalimbali zinazosaidia mwitikio wa Taifa, zikiwemo afua zinazotekelezwa kupitia mpango wa dharura wa Rais wa Marekani wa Ukimwi (PEPFAR).

Waziri Mkuu Majaliwa ametumia maadhimisho hayo ya siku ya Ukimwi Duniani yanayofanyika kila Disemba Mosi, kuzungumzia faida za kampeni ya Furaha Yangu aliyoizindua mwezi Juni mwaka huu ambapo aliagiza mikoa yote kufanya uzinduzi wa kampeni hiyo kwenye ngazi za mikoa na wilaya.

Amesema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo katika mikoa yote nchini, jumla ya wananchi 262,114 walijitokeza kupima ili kujua kama wameambukizwa Virusi vinavyosababisha Ukimwi au la.

Amewahakikishia Watanzania wote kuwa serikali itaendelea kutekeleza na kuboresha huduma za upimaji wa Virusi vinavyosababisha Ukimwi, kuzuia maambukizi ya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, matibabu ya magonjwa nyemelezi na kupiga vita unyanyapaa wa aina zote kwa watu wanaoishi na Virusi vinavyosababisha Ukimwi.