Miradi yazalisha ajira 13,000 miaka miwili ya Rais Dkt. Mwinyi

0
143

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi jumla ya miradi 215 imesajiliwa kupitia Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.26 (shilingi trilioni 7.6).

Waziri Mkuu ameyasema hayo wilaya ya Kaskazini A wakati akizindua hoteli ya nyota tano ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

“Miradi yote hii inatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 13,000,” amesema akiongeza kuwa “mafanikio hayo yamechangiwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Nane zikiwemo sera na mipango madhubuti iliyowekwa na Chama cha Mapinduzi kupitia Ilani yake ya Uchaguzi ya Mwaka 2020.”

Akizungumzia kumbukizi ya mapiduzi amesema ni “sehemu ya historia muhimu kwani zinatukumbusha jinsi ambavyo wakulima na wafanyakazi wanyonge walivyokataa madhila ya kubaguliwa na kunyanyaswa.”

Amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais Dkt. Mwinyi wanao mkakati endelevu wa kukuza sekta ya uwekezaji nchini ikiwemo kushirikisha sekta binafsi nchini na kuvutia mitaji kutoka nje kwa lengo kuhakikisha nchi zetu zinakuwa na uchumi imara.