Miradi Serikali za Mitaa kufadhiliwa kupitia hati fungani

0
295

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kufanya uratibu utakaowezesha mpango ujulikanao kama Municipal Investment Financing, utakaosaidia upatikanaji wa fedha kwa Serikali za mitaa kupitia uanzishwaji wa hati fungani.

Rais ametoa agizo hilo leo mara baada ya kukutana na kuzungumza na Katibu Mtendaji wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Mitaji ya Maendeleo (UNCDF), Preeti Sinha, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo, Bi. Sinha amemueleza Rais Samia kuwa UNCDF ipo tayari kushirikiana na nchi zinazoendelea ikiwa ni pamoja na Serikali ya Tanzania kutafuta njia mbadala za kupata fedha za kugharamia miradi ya maendeleo.

Amesema fedha zitakazopatikana kupitia hati fungani zitarejeshwa kutokana na makusanyo yanayopatikana kwenye Serikali za Mitaa

Kwa upande wake Rais Samia amekubaliana na wazo hilo na kusema kuwa litasaidia kupunguza mzigo kwa Serikali Kuu kuhudumia miradi ya maendeleo ya Serikali za Mitaa.