Mimba za utotoni zaendelea kuwa tatizo

0
253

Ongezeko la mimba katika umri mdogo limeilazimu idara ya elimu ya sekondari wilayani Misungwi, Mwanza kwa kushirikiana na Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Wasichana la Kivulini kuzindua kampeni ya “Kama Unapenda Sketi za Shule Mshonee Mkeo.”

Wanafunzi 84 wa shule za sekondari wilayani humo wamepata ujauzito katika kipindi cha kuanzia Julai 2019 hadi Mei mwaka huu.

Takwimu hizo zimebainishwa na Afisa Elimu Taaluma Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Selema Ikowelo wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo inayolenga kuielimisha jamii ili kutokomeza mimba katika umri mdogo.

Tatizo hili limeendelea kuwa kikwazo kwa watoto wa kike wilayani humo kwa kushindwa kutimiza ndoto zao za kitaaluma.

Kati ya wanafunzi hao, 46 wanaelezwa kupata ujauzito kati ya Januari na Aprili mwaka huu.