Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda imepokea shilingi zaidi ya milioni 900 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya katika kata za Nsemulwa na Kakese kwa lengo la kuwahudumia wananchi zaidi ya 28,000.
Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Dkt Obed Mahenge amesema ujenzi wa vituo hivyo utategemea zaidi nguvu za wananchi kwa kuwa ujenzi utafanyika kwa mfumo wa akaunti ya dharura yaani Force Account.
Amesema wananchi wa Kata ya Kakese wapatao 14,500 na wakazi wa Kata ya Nsemulwa Zaidi ya 13,500 wamekuwa wakipata huduma za matibabu umbali mrefu, jambo ambalo lilikuwa linawapa wakati mgumu wajawazito kuwahi huduma za kujifungua.
Baadhi ya wakazi wa kata hizo wameeleza kufurahi kwao kwa namna ambavyo serikali imesikia kilio chao cha muda mrefu.
Wananchi hao wameahidi kushiriki katika ujenzi kwa nguvu zao, na kuhakikishia majengo ya vituo vya afya yanakamilka kwa wakati.