Baraza la Mawaziri la nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), limekubaliana na ushauri uliotolewa na Mawaziri wa afya wa nchi hizo kuwa mikutano inayotarajiwa kufanyika siku chache zijazo ifanyike kwa njia ya video ikiwa ni moja ya njia za kuepuka maambukizi ya virusi vya corona.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu wa wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Wilbert Ibuge amesema kuwa, Mwenyekiti wa baraza hilo Profesa Palamagamba Kabudi amekubaliana na ushauri huo.
Balozi Ibuge amesema kuwa, kikao cha sekretarieti cha awali kabla ya mikutano hiyo ya Baraza la Mawaziri la nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika kilichokuwa kifanyike kwa muda wa siku tatu sasa kitafanyika kwa muda wa siku mbili na kile cha Mawaziri kitafanyika kwa siku moja.
Kwa mujibu wa Balozi Ibuge, Tanzania ilijiandaa kupokea zaidi ya wageni mia mbili na hamsini kwa ajili ya kushiriki mikutano hiyo, lakini kwa sasa wageni hao hawatashiriki, hatua ambayo imeathiri faida ambazo zingepatikana kwa wageni hao kuwepo nchini.
Ajenda zitakazojadiliwa wakati wa mikutano hiyo ya Baraza la Mawaziri la nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ni pamoja na bajeti ya Jumuiya hiyo, uboreshwaji wa Shirika la Utalii la SADC na masuala ya uchaguzi kwa nchi wanachama zinazotarajiwa kufanya chaguzi mwaka huu.