Dar es salaam, Kilimanjaro na Arusha zafanya vibaya katika uandikishaji

0
209

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo,  amemuomba Rais John Magufuli amkubalie ampelekee pendekezo maalum endapo kutakua na mkoa ambao hautakua umefikisha asilimia Hamsini katika uandikishaji Wananchi kwenye  Daftari la Wapiga Kura mpaka itakapofika  mwishoni mwa zoezi hilo.

Waziri Jafo ametoa ombi hilo wakati wa ziara ya Rais Magufuli mkoani Katavi,  baada ya tathmini ya uandikishaji  iliyofanyika kwa tarehe Nane na Tisa mwezi huu kuonyesha baadhi ya mikoa kufanya vibaya katika uandikishaji.

Amesema kuwa tathmini hiyo inaonyesha  kuwa, katika siku hizo Mbili,  mkoa wa Iringa umeongoza kwa kuandikisha  asilimia  53,  ukifuatiwa na mikoa ya Mbeya, Songwe na Tanga.

Waziri Jafo ameitaja mikoa iliyofanya vibaya ambayo ni Dar es salaam   ambao umeandikisha kwa  asilimia Tano, Kilimanjaro asilimia 12 na Arusha 13.

Amesema kuwa haiwezekani Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ukawa ndio agenda muhimu kwa Serikali na huku kuna watu wanakwamisha kwa makusudi uandikishaji wa Wananchi katika Daftari la Kupiga kura kwa ajili ya uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa Waziri Jafo, haiingia akilini kwa mfano mkoa wa Dar es salaam ambao una viongozi wa ngazi mbalimbali, lakini unafanya vibaya katika jambo muhimu kama uandikishaji Wananchi katika Daftari la Wapiga Kura.

Zoezi la uandikishaji Wananchi katika Daftari la Kupiga Kura kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa lilianza tarehe Nane mwezi huu  na linatarajiwa kukamilika tarehe 14 mwezi huu.